Obama Amteua Msaidizi Wake Kuwa Balozi Tanzania

Obama na Washauri Wake Waandamizi Akiwemo Mark Childress (kulia)
Rais wa Marekani Barrack Obama amemteua msaidizi wake wa karibu, Mark Childress kuwa balozi wa nchi hiyo, hapa nchini.

Childress ni msaidizi wa Obama katika Ikulu ya Marekani (White House) akiwa Naibu Mkuu wa Utumishi anayeshughulikia mipango katika Serikali ya nchi hiyo na aliwahi kufanya kazi katika Bunge la Seneti.


Obama amefanya uteuzi huo ikiwa ni wiki moja tangu alipohitimisha ziara yake katika nchi tatu za Bara la Afrika, Tanzania ikiwa mojawapo. Pia alizitembelea Senegal na Afrika Kusini.

Hata hivyo, taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Marekani jana ilisema nafasi hiyo inahitaji kuidhinishwa na Bunge la Seneti la nchi hiyo. Uteuzi wake unaweza kuwa na maana kubwa katika kutekeleza sera za nje za Marekani.

Katika miaka ya karibuni, Tanzania imeshuhudia ziara za viongozi wakuu wa nchi hiyo nchini ambao ni Bill Clinton, George Bush na Obama.

Kuteuliwa kwa Childress, kunaashiria kwamba Balozi wa sasa wa Marekani nchini Alfonso Lenhardt anakaribia kumaliza muda wake.

CHANZO: Gazeti MWANANCHI

No comments:

Post a Comment