Rostam Aziz Ndiye Tajiri Namba Moja Tanzania Awapiku Bakhresa, Mengi na ‘Mo’

Rostam Aziz
Mfanyabiashara maarufu nchini, Rostam Aziz (49), ametajwa kuwa ndiye tajiri namba moja Tanzania kwa sasa.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Jarida la Marekani la Forbes na kutoa taarifa yake juzi, Rostam amekamata nafasi hiyo na ya 27 katika Afrika akiwa na utajiri wa Dola za Marekani bilioni moja (Sh1.6 trilioni).

Mbunge huyo wa zamani wa Igunga, ameingia kwa mara ya kwanza katika orodha ya matajiri 50 wa Afrika ya jarida hilo, pamoja na wafanyabiashara wengine wa Tanzania, Reginald Mengi na Mbunge wa Singida Mjini (CCM), Mohamed Dewji ‘Mo’. Katika orodha hiyo pia yumo Said Bakhresa ambaye aliwahi kutajwa siku za nyuma.

Rostam, ambaye aliachana na siasa mwaka 2011, amempiku Bakhresa, ambaye mwaka jana Jarida la Ventures Africa la Nigeria lilimtaja kuwa ndiye aliyekuwa tajiri namba moja wa Tanzania. Bakhressa katika kipindi hicho alikadiriwa kuwa na utajiri wa Dola 620 milioni (Sh971 bilioni).

Katika orodha hiyo ya Ventures Africa, Bakhresa alifuatiwa na Rostam, Mengi na mfanyabiashara mwingine maarufu, Ali Mufuruki.

Mengi anashika nafasi ya pili kwa Tanzania na ya 34 Afrika akiwa na utajiri wa Dola 550 milioni (Sh861 bilioni).

Forbes linaonyesha kuwa Bakhresa amefungana na Mo katika nafasi ya tatu ya orodha ya matajiri wa Tanzania na ya 38 kwa Afrika, wote wakiwa na utajiri wa Dola 500 milioni (Sh783 bilioni).



Rostam Aziz

Jarida la Forbes limeripoti kuwa utajiri wa Rostam unachangiwa zaidi na biashara ya mawasiliano ya simu za mkononi, ujenzi na uchimbaji wa madini.

Anamiliki asilimia 35 ya hisa katika Kampuni ya Simu za mkononi ya Vodacom. Ni kampuni inayoongoza kwa biashara ya simu za mikononi nchini Tanzania ikiwa na wateja zaidi ya milioni 9.5.


Listi ya Matajiri 10 Wanaaongoza kwa Utajiri Barani Afrika




KWA UFUPI:

Jarida la Forbes lamtaja Rostam kuwa ni namba moja,
akifuatiwa na Mengi, Bakhresa na Mo.
Wamo katika orodha ya matajiri 50 wa Afrika
wakiongozwa na Dangote wa Nigeria

CHANZO: Gazeti Mwananchi

No comments:

Post a Comment