Laptop Ilichangia Mauaji ya Kutisha Ilala Bungoni [HABARI KAMILI]

Kwa ufupi
  • Desemba mwaka jana ni wakati, Gabriel Munisi alipokutana na Christina Newa. Awali lilikuwa penzi, ambalo Christina aliamini litampa faraja na kuyabadili maisha yake. 
  • Hata hivyo, ndoto yake hiyo ilibadilika muda mfupi tu wa penzi hilo baada ya mpenzi wake, Munisi, kuanza kuonyesha ukali uliopitiliza, wivu na maneno makali.
Yumkini wengi wanapotamka neno ‘penzi’ lenye herufi tano tu, hudhani ni dogo lisilo na uzito katika maisha ya binadamu.

Lakini kama umeshawahi kusikia kuwa mapenzi yanaua, basi uhalisia unaoonyesha  madhara, uzito na machungu ya mapenzi...ndiyo huu hapa.

Desemba mwaka jana ni wakati, Gabriel Munisi alipokutana na Christina Newa. Awali lilikuwa penzi, ambalo Christina aliamini litampa faraja, kicheko na kuyabadili maisha yake.

 Hata hivyo, ndoto yake hiyo ilibadilika muda mfupi tu wa penzi hilo baada ya mpenzi wake, Munisi, kuanza kuonyesha ukali uliopitiliza, wivu na maneno makali.

 “Gaby alikuwa anaishi kwa kasumba, hajiamini, mkorofi na aliyependa kunitishia kwa kutumia silaha mara kwa mara,” anasema Christina.

Ukali wa Munisi haukupungua licha ya Christina kujaribu kumbadili hata kumshauri aonane na daktari wa masuala ya saikolojia ambaye anaweza kumtibu.

 “Nilimwona si wa kawaida. Nilipomshauri kuhusu tiba, alikubali na akampigia simu daktari mmoja aliyekuwa hospitali ya Bugando ambaye alikubali kuwa, inawezekana Gaby ana matatizo ya kisaikolojia na wakakubaliana kuwa ataanza tiba,” anasema.

Christina baada ya kuona penzi lake na Munisi limekithiri kwa  misuguano, mifarakano na vitisho, alishauriana na familia yake, kisha wakaamua kuwa aende kusoma katika Visiwa vya Cypruss, ili kujiongezea maarifa lakini pia atakuwa mbali na Munisi ambaye alikuwa sasa anaonekana kuwa tishio.

Munisi alionekana kuwa tishio mara baada ya kumtakia hadharani Christina kuwa endapo atamchezea ataisambaratisha familia yake akianzia na Goba, anakoishi mama yao, Ellen Eliezer, kisha Zanzibar anakoishi mdogo wake, Alpha Newa na kumalizia Ilala, inakoishi familia hiyo.

Kwa maelezo ya Christina, kosa kubwa ambalo lilionyesha kumuudhi zaidi Munisi, ni kitendo chake cha kuondoka nchini bila kumuaga. Hata hivyo Munisi hakukata tamaa bali alihakikisha anapata mawasiliano ya Christina akiwa huko visiwani Cypruss.

“Tuliwasiliana tukiwa kule na tukazungumza. Kwa sababu ilikuwa  ni kipindi cha likizo akaniambia atakuja kunipokea uwanja wa ndege. Nilidhani atakuwa amebadilika kwa kipindi hiki,” anasema.

Cha ajabu, Munisi baada ya kumpokea Christina, alimkataza kwenda nyumbani kwao na badala yake alimlazimisha waende, Mwanza, Kitangiri, anakoishi.


Alimchukua moja kwa moja na kumkataza hata kwenda kuisabahi familia yake, na siku ile ile safari ya kuelekea Mwanza ilianza. Lakini usiku wa manane wakiwa katikati ya safari, Munisi alifanya jambo la kushangaza.

“Alisimamisha gari maeneo ya Singida na kunitaka nishuke. Niliposhuka, alitoa bastola akaniambia kwa nini niliondoka bila kumuaga au nataka kumuacha?” anasema na kuongeza: “Kitendo kile kilinitisha kwa sababu sikutegemea kama angenishusha usiku ule porini namna ile na kutoa bastola.”

Laptop ilichagiza mgogoro


 Walipofika Mwanza, Munisi alimfungia ndani Christina, lakini alichukua simu zake zote mbili pamoja na laptop ambavyo ilivifanyia uchunguzi wa kina.

Christina anaeleza kuwa Munisi aliipeleka laptop kwa wataalamu wa teknolojia, ambao walimsaidia kuifungua (ilikuwa ikitumia namba ya siri) na alianza kupekua taarifa zote zilizomo. “

Alikuta baadhi ya picha zangu ambazo nilizituma ‘facebook’. Picha hizo ni za ufukweni ambazo nilipiga na wenzangu  huko Cypruss. Nilikuwa nimevaa nguo za kuogelea na ndiyo jambo lililomkera,” anasema.

 Anasema baada ya kuona picha hizo, alimgombeza na kumpiga kiasi cha kumuumiza kwenye magoti na ndipo alipozidisha ulinzi katika nyumba yake.

Inaelezwa kuwa Munisi alibaki na laptop ya Christina ambayo alikuwa akitembea nayo na kuwaonyesha watu picha za mpenzi wake huyo na kusema:

“Unajua mi nilitaka kumuoa huyu, lakini angalia picha anazopiga, ungekuwa wewe ungefanyaje?”

Lakini Christina alijitetea kuwa hilo si jambo la ajabu katika familia yao kwani hata akiwa nyumbani huvaa hivyo.

Anapanda dirishani kuomba msaada

Baada ya kuona anaendelea kufungiwa ndani bila mawasiliano ya aina yeyote, alichukua uamuzi wa kupanda dirishani na kuwaita wapita njia ili wamsaidie


Mama mwenye nyumba hiyo pamoja na watoto walimsaidia Christina kwa kuwapigia simu ndugu zake na kuwaeleza matatizo anayoyapata. “Mama mwenye nyumba aliniambia kuwa wanawake zaidi ya 30 walioishi na Munisi, walikuwa wakipitia matatizo kama hayo niliyopitia mimi,” anasema.

 Anaondoka Mwanza na ulinzi wa polisi

 Baada ya ndugu zake kupambana, ilibidi polisi watumie ujanja na kumdanganya Munisi kuwa aende kituo cha polisi kwani kuna biashara (dili) ya magari.

Hata hivyo, Munisi alitia shaka na akaamua kwenda na Christina huko polisi, ambaye alikuwa amevaa khanga na fulana tu.

 Ingawa Christina alimbembeleza Munisi aingie chumbani kuvaa, lakini hakuruhusiwa hata kidogo.

Walipofika polisi, simu ilipigwa na wazazi wa Christina wakamtuma ndugu yao ainayeishi  Mwanza,(alifahamika kwa jina moja la Mpangala) ambaye alisaidia kumrudisha Dar es Salaam.

Nyendo za Munisi

 Baada ya Christina kurudi Jijini, Munisi alianza nyendo za kushangaza ambazo pengine ndizo zilizosababisha maafa haya.  Munisi alipanga katika hoteli ya M.M. ambayo ipo karibu kabisa na nyumbani kwa Christina, Ilala Bungoni. Akiwa hapo alikuwa akifuatilia maisha ya wanafamilia hao.

“Nilijua anatufuatilia kwa sababu alikuwa akinitumia meseji kunieleza kila tulichokuwa tunafanya na ndugu zangu. Nahisi pia alikuwa na mtu anatupeleleza,” anasema

 Siku moja Christina akiwa kituo cha mabasi cha Amana, alihisi mtu amemshika bega, alipogeuka alishangaa kumwona Munisi.

“Nilitetemeka na kutamani kupiga kelele, lakini alinitoa hofu na kuniambia ananipenda, hivyo twende pembeni kuzungumza,” anasema.

 Walitafuta eneo wakaketi na kuanza mazungumzo ambapo hata hivyo Christina hakuwa na amani tena na mwanaume huyo.


Maafa yanatokea

Siku ya tukio, Christina, mama yake, mdogo wake, Alpha  pamoja na shemeji yake, mume wa dada yake, marehemu  Francis Shumila walikuwa katika gari wakielekea uwanja wa ndege.

“Wakati gari linatoka getini, tulimwona Munisi akivuka barabara kwa kasi, akija upande wetu. Nilijua anakuja kufanya jambo baya,” anasema.

Shumila ambaye aliufahamu fika ugomvi huo, alishuka kwenye gari ili akamsihi Munisi asimdhuru Christina, lakini Munisi bila kuchelewa alimmiminia risasi zaidi ya tano kichwani.

“Risasi zilimuishia, akaweka nyingine kisha akaenda upande aliokaa Alpha na kumpiga za kifuani,

kisha akaanza kutumiminia mimi na mama,” anasema.Shumila, alifariki dunia siku moja baadaye, Alpha alikufa palepale, wakati Christina na mama yake walijeruhiwa.

Hata hivyo Caroline Newa, dada yake Christina, ambaye ndiye mke wa marehemu Shumila, anasema polisi walipewa taarifa za vitisho vya Munisi lakini hawakutilia maanani.

“Tulitoa taarifa zaidi ya mara nne, lakini polisi walitudhalilisha wakatuambia hayo ni mambo ya mapenzi tu,” anasema Caroline.

Walibembeleza angalau kupewa hati ya taarifa(RB) lakini polisi walikataa katakata.

Shumila alijitabiria kifo

Caroline, anasema, siku chache kabla ya tukio hilo, Shumila, ambaye ni mume wake, alimtoa hofu Christina na kumwambia kuwa atamlinda kwa gharama yeyote ile hata kama kupoteza maisha yake.

“Kwa kuwa alikuwa akijua historia yote ya mfarakano huu, alimwambia Christina asiwe na wasiwasi atamlinda na kweli ndivyo ilivyotokea” anasema Caroline.


CHANZO: Gazeti MWANANCHI

No comments:

Post a Comment